BREAKING NEWS: Loading latest posts...

Sunday, July 5, 2026

WADAU WA SEKTA YA MADINI WATAKIWA KUFANYA TAFITI ILI KUONGEZA UZALISHAJI WA MADINI


Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam,


Wachimbaji wadogo wa madini wamehimizwa kufanya tafiti za madini kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa madini, kuepuka hasara na kuongeza uzalishaji pamoja na mapato.

Rai hiyo imetolewa leo, Julai 5, 2026, na Mjiolojia Mkuu kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Bw. Hamis Ramadhani, wakati akitoa elimu kwa wachimbaji wa madini waliotembelea banda la GST katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Bw. Hamis amesema wachimbaji wadogo wengi bado wanaanza shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia na kijiosayansi kuhusu maeneo wanayochimba, hali inayochangia kupata kiwango kidogo cha madini au kutopata madini kabisa, na hivyo kupoteza muda, nguvu na mitaji yao.

"Upatikanaji wa madini ni suala la kisayansi. Wachimbaji wadogo wanapaswa kutumia huduma za GST ili kufanyiwa tafiti katika maeneo yao. Kupitia tafiti hizo, wataelekezwa kama eneo lina madini na mwelekeo wa mwamba (mbale) unaobeba madini hayo," amesema Bw. Hamis.

Aidha, ameeleza kuwa GST inamiliki maabara ya kisasa ya uchenjuaji wa madini inayowezesha kufanya uchunguzi wa mbale na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu njia bora za uchenjuaji kulingana na sifa za madini yaliyopo.

Amefafanua kuwa baadhi ya wachimbaji hupoteza sehemu kubwa ya madini wakati wa uchenjuaji kutokana na kutotumia teknolojia na mbinu sahihi, ikiwemo kiwango stahiki cha kusaga miamba yenye madini na matumizi sahihi ya kemikali katika mchakato wa uchenjuaji.

Bw. Hamis amesema kupitia Maonesho ya Sabasaba, GST inaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji na wadau wa sekta ya madini kuhusu umuhimu wa kutumia matokeo ya tafiti za kijiolojia katika utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kuongeza uzalishaji, tija na mapato.

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Madini yenye jukumu la kufanya tafiti za jiolojia na madini nchini, pamoja na kuhifadhi taarifa rasmi za rasilimali za madini kwa niaba ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages